top of page
Search

Tuwekeze Katika kuwainua wasichana

Mariam Mmbaga

Tuwekeze Katika kuwainua wasichana ili kujenga wanawake bora wa baadae

Tarehe 8 ya Mwezi Machi taasisi ya Tai Tanzania iliungana na ulimwengu mzima kusherekea siku ya wanawake duniani, ambayo ni siku maalumu iliyotegwa kusherehekea mafanikio ya wanawake katika Nyanja za uchumi, siasa utamaduni na jamii kwa ujumla, sherehe ilifanyika katika shule ya secondari ya Salma Kikwete.

Tai ilichukuwa fursa ya kipekee kuadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kuwaalika wanaharakati wa wanawake kuzungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari hasa wakike,kwakuwa inaamini kwa kumuinua mtoto wa kike leo, ni sawa na kumuinua mwanamke wa baadae.

Kwa kutambua mchango wa wanawake katika jamii Taasisi ya Tai ilimualika Mama Valerie Msoka ambae ni Mwenyekiti wa Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania, kama mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho hayo, pia Tai iliwaalika wageni wengine ambao ni wanaharakati wenye mchango mkubwa katika kumuinua mwanamke katika jamii akiwemo Richard Mabala ambae ni mwandishi wa vitabu mashuhuri kama “Mabala the famer”, “Hawa the bus driver”, na Elizabeth Ndakidemi ambae ni naibu mkurugenzi wa Taasisi ya TAYOA.

Mama Valerie Msoka ni moja kati ya wanawake walioweza kubadilisha changamoto kuwa fursa za maendeleo, aliwahamasisha wasichana kwa kuelezea uzoefu wake katika tasnia ya habari alisema kipindi anaanza kazi akiwa kama mwanahabari, habari zilizoandikwa na wanawake hazikuwa na nafasi ya kuchapishwa, hilo likapelekea kuanzisha umoja wa waandishi wa habari wanawake (TAMWA)ili kuweza kupaza sauti zao juu ya changamoto wanazozipitia kama wanawake kwenye tasnia ya habari,umoja huo umesaidia sauti nyingi za wanawake kuweza kusikika na hatimae kuleta maendeleo kwenye tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Richard Mabala alionesha umuhimu wa mwanamke katika jamii kwa kutolea mfano wa namna vitabu vyake vilivyo muonesha mwanmke kama mtu mwenye ujasiri na ushupavu, pia alitoa mfano wa filamu mashuhuri ya Sarafina “Mama yake Sarafina aliteswa, akanyanyaswa na kudharauliwa lakini alivumilia kufanya kazi hiyo ili aweze kumpatia maisha mazuri mwanae, hivyo katika maisha yetu ya kila siku ni lazima tukumbuke mchango wa mama na dada zetu, uvumilivu wao na mabapano yao ndio yanatufanya tuwe hapa leo”.

Taasisi ya Tai Tanzania inaunga mkono kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani “Wakati ni sasa wanaharakati wa mjini na vijijini kubadilisha maisha ya wanawake” kwa kuhakikisha wasichana wanabaki shule kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi ili kuwaepusha na mimba za utotoni, pamoja na taulo za kike ili waweze kujistiri wakati wa siku za hedhi na kuhudhuria masomo yao kikamilifu,Tai inalengo la kupelekea elimu zaidi maeneo ya vijijini ambapo matatizo yanayowakumba wasichana ni mengi zaidi.

“Tumesherekea siku ya wanawake duniani kwa kuzungumza na wanafunzi wa shule za secondary hasa wasichana kwakuwa ni wanawake watarajiwa , wasichana wanatakiwa kufundishwa na kuhamasishwa nini wafanye ili waweze kujijengea msingi mzuri wa maisha ya baadae, waweze kuamini kuwa wao ndio chachu ya maendeleo katika jamii inayowazunguka” alisema Asimwe Rutageruka, Meneja wa mradi wa Jali kutoka Tai.

Wanafunzi pia waliweza kuburudisha na kufikisha ujumbe kwenye jamii kupitia kuimba shairi lililoandaliwa na Taasisi ya Tai kwa lengo la kuwawezesha wasichana kuzifahamu haki zao ndani ya jamii.

Elimu ya Afya ya uzazi ikatolewa na Daktari Joseph Lori, kutoka hospitali ya Tumaini, pia timu ya Madaktari kutoka TAMHEF ikatoa huduma nzuri ya wanafunzi kupima afya zao “Ni vyema wanafunzi kujua hali ya afya zao ili waweze kuhudhuria masomo yao kwa ukamilifu, hivyo tumeleta huduma hii kwa wanafunzi kwakuwa wengi wao hawatoi kipaumbele cha kupima afya zao”alisema daktari Juliana Busasi kutoka TAMHEF .

Video fupi ya Harakati za Lucy https://www.tai.or.tz/harakati-za-lucy inayolenga kuibua changamoto anazopitia mtoto wa kike kipindi cha hedhi ilipata nafasi ya kutazamwa na kufurahiwa na wanafunzi, pia video zilizoandaliwa na Taasisi ya Her Cause Foundation zenye lengo la kumuelimisha mtoto wa kike.

Wanafunzi wakapata fursa ya kuandika ujumbe mahususi kwa ajili ya siku ya wanawake duniani, unaolenga kutambua umuhimu wa kuzitambua haki zao na mafanikio ya wanawake kwenye jamii inayowazunguka.

Kuna msemo unasema “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako” Taasisi ya Tai inalengo la kwenda mbali ndio maana ilishirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kufanikisha sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawae duniani, kwa kufikisha ujumbe mbalimbali wenye lengo la kuwahamasisha wanafunzi hasa wale wa kike kuweza kujiamini na kuepuka kujiingiza kwenye mambo ambayo yanaweza kuwafanya wasifikie malengo yao, Taasisi ya Tai inatarajia kueneza elimu zaidi kupitia njia mbalimbali ikiwemo ya kufanya matamasha kwenye jamii.

53 views0 comments

Recent Posts

See All
  • YouTube
  • Facebook Social Icon
  • Instagram
  • Twitter Social Icon
bottom of page